Swali: Jina Said
Ahmed Mohammed ni jina kubwa sana katika fasihi ya Kiswahili. Wasomaji
wangependa kumfahamu mtu huyu. S.A.M. ni nani?
Jibu: Mimi ni binadamu wa kawaida. Nilizaliwa Pemba, mnamo Tarehe 12 Disemba 1947. Nilijiunga na shule ya Msingi ya Darajani ambayo iko Zanzibar mjini na baadaye nikaendelea na masomo yangu ya /sekondari katika Shule ya Upili ya Gulioni iliyokuwa kitambo ikiitwa King George the VI. Baadaye nilijiunga na chuo cha ualimu cha Nkrumah TTC, mjini Zanzibar mwaka wa 1966.
Nilipofuzu chuoni nilifundisha shule
ya Msingi ya Kizimbani kwa wiki mbili tu halafu nikahitajika kuenda
kufundisha Shule ya sekondari ya Utaani baina ya 1969 na 1974. Nilikuwa
nikifundisha masomo ya Biolojia, Hesabu na Kemia na pia Kiswahili. Kwa
kuwa nilikuwa bado nikiandika hadithi fupi zilizosomwa katika vituo vya
BBC na DW Welle, hapa ndipo nilipopata wazo la kuandika Asali Chungu.
Baadaye nilijiunga na kidato cha 5
na 6 (A-level) nikipanga kuendelea kufanya masomo ya sayansi.
Palikosekana vifaa vya kufanyia masomo ya utekelezi wa kisayansi (practicals) na hivyo nikachagua kufanya masomo ya kisanaa.
Swali:
Kwa hivyo Profesa ungepata shule yenye vifaa hivyo, tungekuwa na Said
Ahmed Mohammed mwanasayansi na labda Kiswahili kingekosa mwandishi kama
wewe.
Jibu: (Kicheko)Aaah! Sidhani hivyo.
Uandishi umekuwa katika damu yangu tangu utotoni. Hujaona watu
wanaoandika na bado ni wanasayansi au wanafanya kazi tofauti? Kwa mfano
kuna Daktari Yusuf Dawood n.k. Mimi nilipenda kusoma na kutunga mashairi
na hadithi fupi. Hata hadithi zangu zilisomwa redioni katika idhaa za
BBC-Swahili, DW welle.
Nilipokuwa darasa la tano mashairi
yangu yalitumiwa na walimu katika kuchambua na kufundishia madarasa ya
juu. Nilifanyiza kazi talanta yangu.Nafikiri bado ningekuwa mwanasayansi
mwandishi. Nashukuru Mungu nilifanya vyema katika kila somo.
Swali: Ni lini ulipojiunga na chuo kikuu na uliendeleaje?
Jibu: Mnamo 1976 nilijiunga na Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam kusomea shahada ya kwanza ya BA katika
Elimu-nikimakinikia Isimu na Fasihi ya Kiswahili. Baada ya kufuzu katika
shahada hiyo nilirejea nyumbani Zanzibar na kuwa mwalimu mkuu wa Shule
za Msingi na Upili za Hamamni kwa miaka mitatu. Nilikuwa na wasaidizi
kama watatu hivi kila moja akiwa na kiwango maalumu cha kusaidia kama
shule ya Msingi, ya upili, utawala na kadhalika.Nilirudi tena Chuo kikuu
cha Dar es Salaam na kujisajili kusomea shahada ya Uzamili yaani MA
katika Isimu tekelezi nilipoangazia kazi za mwenzangu Mohammed Said
Mohammed.
Nilipokuwa nikisoma hapa, kipawa
changu kilimvutia mwalimu wangu wa kutoka Ujerumani aliyefundisha Isimu
linganishi na ya Kihistoria Bw.Sigmund Brauner. Hapa ndipo fursa ya
kuelekea Ujerumani kufanya shahada ya Uzamifu yaani PhD na pia
kufundisha ilipotokea. Nilijiunga na Chuo Kikuu cha Karl Marx Leipzig
hapa Ujerumani mwisho wa mwaka wa 1981 na kukamilisha mwaka 1985.Sasa
nikawa Daktari. Hapa nilikuwa pamoja na familia yangu.
Swali: Ulipokamilisha shahada hii muhimu, ulibakia Ulaya kufundisha?
Jibu: La hasha! Niliteuliwa na Rais
wa Zanzibar wakati huo Mzee Idris abdul Wakil na kurejea nyumbani
Zanzibar na kuwa Mkurugenzi wa pili wa Taasisi ya Kiswahili na Lugha za
Kigeni (TAKILUKI) baadaye iliyokuwa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) kwa
miaka miwili. Niliondoka kwa sababu za kisiasa na fitina za watu ambao
sikuwafahamu.
Baadaye nilienda Kenya mnamo 1987 na
kuwa mwenyekiti wa kwanza wa Idara ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha
Moi mjini Eldoret na baadaye kufundisha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha
Nairobi, ndaki ya Kikuyu hadi mwaka wa 1990. Nilipotoka Nairobi
nilielekea Japan katika Chuo Kikuu cha Osaka idara ya lugha za kigeni.
Nikiwa Japan ndipo nilipata uprofesa. Nilipotoka Osaka, Japan ndipo
nikaja hapa Chuo Kikuu cha Bayreuth tangia 1997 hadi wa sasa nafundisha
hapa.
Swali:
Wengi wamekutaja kama mwandishi mashuhuri zaidi Afrika Mashariki na
hata Afrika nzima ukiwa umeweza kuandika riwaya, tamthilia, mashairi,
kazi za watoto na hata vitabu vya shule na vyuo. Je, umeandika vitabu
vingapi?
Jibu: Vingi tu! Nafikiri nimeandika
vitabu zaidi ya hamsini na vitano (55). Kuna vya Mashairi kama Sikate
Tamaa (1980), Kina Cha Maisha (1984), Jicho la Ndani (2002), na
tamthilia kama Pungwa (1988), Kivuli Kinaishi (1990), Amezidi (1995),
Kitumbua Kimeingia Mchanga (2000), pamoja na rafiki yangu Prof.Kitula
King’ei tumeandika Posa za Bi Kisiwa (2007), na riwaya kadha kama vile
Asali Chungu-1977, Utengano-1980, Dunia Mti Mkavu-1980, Kiza katika Nuru
1988,Tata za Asumini 1990, Babu alipofufuka-2001,Dunia Yao- 2006, na
ya majuzi zaidi Nyuso za mwanamke- 2010 na vingine kadha. Baadhi ya kazi
zangu zimetafsiriwa kwa lugha za kigeni pia.
Pia kuna miswada ambayo itachapishwa
hivi karibu ya riwaya ya Mkamadume, Mhanga nafsi yangu na kitabu cha
kusomwa katika darasa la saba hivi kiitwacho Gharama ya Amani
kiachoangazia fujo za kisiasa zilizotokea Kenya.
Swali: Ni gani miongoni mwa
hivi vyote kwa maoni yako unachofikiria ni kitabu maarufu zaidi au
unachokipenda kuliko vyote ulivyowahi kuandika?
Jibu: Wewe si wa kwanza kuniuliza
swali hilo. Nitasema kuwa kazi za uandishi ni kama watoto wangu. Siwezi
nikakwambia nampenda huyo na simpendi huyo mwingine. Lakini nafikiri
Nyuso za Mwanamke (2010) ni riwaya ambayo ilinipeleka mbele sana kama
mwandishi na kunipa ujasiri zaidi. Pia wachapishaji wananiambia vile
kuinavyonunuliwa na vile kinavyorudiwa kutolewa Nakala haraka ni ishara
ya kuwa kinasomwa sana. Hata yasemwayo na wahakiki ni muhimu kwangu.
Swali: Je, nini maoni yako kuhusu mchango wa Muungano wa Afrika Mashariki katika kukuza lugha ya Kiswahili?
Jibu: Kila siku nasema kuwa hakuna
njia ya kukiua Kiswahili? Wapo watu wanaodhania kuwa lugha zao
zinawafaa zaidi kiuchumi na wanafikiri Kiswahili hakiwezi baadhi ya
mambo.Kiswahili kinaweza kutumika na muungano huu kufungua nafasi za
kiuchumi.
Kiswahili ni nyenzo ya kiuchumi na
sio kisiasa. Hasa kikienda pole pole kwenye mitaala na kufundishia
masuala ya kitaaluma. Nimesafiri Japan, China, Korea na nimeona mantiki
ya jambo hilo. Wamepiga hatua kubwa kimaendeleo kutumia lugha zao. Nani
kasema sayansi ni ya Kingereza au Kifaransa tu? Nafikiri pale Tanzania
ilipokosea ni pale ilipokuza Kiswahili tu na kupuuza alichokiita Mwalimu
Nyerere-Kiswahili cha Dunia- alimaanisha Kingereza. Ni bora kushika
zote ili tuweze kupiga hatua.
Nchini Kenya, hali ni tofauti kwani
walishika Kiingereza na sasa wameweka mikakati ya kukuza Kiswahili kama
lugha rasmi. Muungano uibuke na sera bainifu za lugha ya Kiswahili na
kuzioanisha katika Baraza la Kiswahili la Afrika Mashariki.
Swali:
Nashukuru kuwa ulimakinikia wasilisho langu kuhusu Swahilihub. Je,
unafikiri tovuti kama yetu ina fursa gani katika kueneza Kiswahili kote
ulimwenguni?
Jibu: Mwanzo ni muhimu watu watambue
kuwa hili ni jambo kubwa sana ambalo Shirika la Nation Media limefanya
na mtaona uzuri wake. Si jambo dogo. Pili, ifahamike kuwa njia ya
kiteknolojia au kidijitali ndiyo ya kipekee katika karne hii ya kuweka
lugha katika kila medani. Hatua yenu ni taji kwa Kiswahili. Nawapa
hongera tovuti ya www.swahilihub.com
Swali: Je, Profesa una familia?
Jibu: Ndiyo. Yupo mke wangu Rahma
nimpendaye na watoto wetu wawili, msichana na mvulana. Binti anaitwa
Najima jina linalomaanisha nyota. Naye bwana mdogo aitwa Mahir- neno la
Kiarabu kumaanisha mwenye ujuzi. Wote wamekamilisha masomo ya shahada ya
kwanza. Najima anajipanga kuendeleza masomo yake naye Mahir ataka
kupata kazi mwanzo. Tunashukuru Mungu.
Swali:
Leo unastaafu kutoka Chuo hiki cha Bayreuth baada ya kufundisha kwa
miaka 13. Unaelekea wapi sasa na je, ulitimiza uliyoyalenga hapa?
Jibu: Inshallah, mimi narudi
nyumbani Zanzibar yaani kwangu Pemba ili niweze kuketi na kutulia
nikilenga kupanua nafasi za kiubunifu katika maandishi. Hapa nitaweza
kuandika niliyoyawazia kwa kuwa muda utakuwepo sasa. Hapa Bayreuth,
nimekuwa na malengo ya chuo na ya Kibinafsi. Alhamdulilahi, yote
yametimia.
Upande wa chuo, nimekuwa Profesa wa
Fasihi za Kiafrika katika Lugha za Kiafrika na hakuna profesa mwingine
katika eneo hilo Uropa nzima. Pia nimegundua kuwa zipo fasihi nyingi tu,
ila mimi nimekuwa balozi wa aina hiyo ya fasihi huku Ulaya. Kazi zangu
zinaenda sambamba na za mwandishi mashuhuri wa Ujerumani Günter Wilhelm
Grass.
Pia nimewashauri wanafunzi wengi wa
Phd kutoka Kenya na kwingineko. Aidha nimeingiza somo la nadharia na
kuamsha usomi wa wanafunzi hapa chuoni na hata kuweza kulinganisha
fasihi za Afrika Mashariki na Afrika Magharibi.
Kwa upande wangu, nimesoma mwenyewe
na kufungua macho yangu kuhusu mambo ambayo nisingeweza hata
kuyafikiria. Kuwa kwangu hapa kumenijifunza uhusiano wa kimataifa,
kufikiriana, kusaidiana na kutoana unyama uletwao na kudhulumiana.
Nawashauri vijana waangalie watu katika jamii walio vilelezo bora na
wafuate nyayo zao kwa kufanya bidii na kujitolea. Vijana waunge mtandao
na wasomi wengine wanaoweza kuwashika mkono maishani.
Bw.Gikambi ni Meneja wa Mradi wa Swahilihub
hgikambi@ke.nationmedia.com
No comments:
Post a Comment