Friday, 21 April 2023

KAWEGERE: MWANDISHI WA ‘SHAMBA LA WANYAMA’ BADO ANATETEA HAKI

 

KAWEGERE, MWANDISHI WA  ‘SHAMBA LA WANYAMA’ BADO ANATETEA HAKI

Na Hezekiel Gikambi akiwa Bukoba, Tanzania, Agosti 2013

Katika Kongamano la hivi majuzi la kumbukumbu la miaka 50 la kumuenzi mwandishi mashuhuri wa riwaya na mashairi marehemu Sheikh Shaaban Suleiman Ufukwe Bin Roberts almaarufu Shaaban


 Roberts mjini Bukoba Tanzania, nilikutana na mwandishi mwengine maarufu sana. Huyu si mwingine bali ni Bw.Fortunatus Felix Kawegere aliyetafsiri na kuifasiri riwaya iliyoibukia kupendwa sana ya Shamba la Wanyama kutoka kwa riwaya asilia ya Mrusi George Orwell ya Animal Farm.

Wasomaji wa kazi zako hasa riwaya maarufu Shamba la Wanyama wangependa kukufahamu zaidi.

Nilizaliwa tarehe 08/04/1943 hapa mjini Bukoba mkoani Kagera nchini Tanzania na kusomea katika shule ya Msingi ya Bunena baina ya mwaka wa 1950- 1954 na kuendelea na Shule ya Kati ya Kitejagwa –kama ilivyoitwa enzi hizo. Baadaye nilijiunga na Chuo cha Ualimu cha Kijunguti baina ya mwaka wa 1960-1961. Tarehe hiyo inakuambia kuwa nilikamilisha kozi ya ualimu wakati Tanganyika inapata uhuru wake.

Masomo yako yalikomea hapo au ulijiendeleza zaidi?

Niliamua kupiga hatua mwenyewe kimasomo kwa kujisajili na vyuo vilivyotoa masomo kwa njia ya posta vilivyoitwa ‘Rapid Results’ kati ya mwaka 1960-1963. Nilichukua somo la Lugha ya Kiswahili, Uchumi na Biashara. Kwa kweli nilimakinikia somo la Kiswahili kwa kuwa nimekuwa nikiipenda sana lugha hii. Napenda chochote kinachomtambulisha mtu yeyote na kukuza utamaduni wake. Hapo ndipo mbegu ya uandishi ilipoatikwa na ikamea na kuzidi kupaliliwa na mapenzi yangu kwa Kiswahili.

Ulianza lini  kazi ya uandishi wako na uliiendelezaje?

Nilisoma riwaya ya George Orwell ya Animal farm mwaka wa 1964 na ikanichochea sana. Niliona kama inamulika na kuakisi uhalisia katika jamii yetu kwa kiwango kikubwa mno. Nilipata mshawasha wa kuifasiri riwaya hiyo kwa Kiswahili mwaka wa 1965 ili ujumbe uliokuwemo uwafikie wananchi wa Tanganyika na Afrika Mashariki kwa jumla. Kilichapishwa mwaka wa 1967. Kabla  ya hapo nilikuwa tayari nimeandika riwaya ya Kiingereza ya upelelezi iitwayo-Inspector Rajabu investigates. Nilipokuwa Mwalimu, Wizara ya Elimu pia iliniita Chuo cha Walimu cha Kiburunyembe, Morogoro  kushiriki katika kuandika kitabu cha wizara cha kozi ya mafunzo ya Kiswahili kilichoitwa Tujifunze Lugha Yetu. Sura tatu nilizoandika kama vile Gulio la Katerero, Mbunge wetu, ziliibukia kupendwa sana. Hapo nikajitoza kikamilifu katika uandishi.  Nimeandika vitabu vingine kama vile riwaya ya Kinga ya Rushwa, diwani ya Mashairi ya Kazi yangu, Uongo uliozaa jitu, Sayari iliyozama, Mgeni wa Usiku na vya  Kiingereza kama Flying without Wings, A Narrow Escape na A Dancing Boat. Ninaendelea kuandika.

Serikali changa ya Tanganyika ilichukuliaje riwaya ya Shamba la Wanyama inayosawiri viongozi wanaowadhulumu raia wake?

Kwa sadfa kubwa, riwaya ya Shamba la Wanyama ilipotoka mwaka wa 1967, ndipo Azimio la Arusha lilipopitishwa na kuzinduliwa rasmi. Azimio  hilo lilikuwa kama ramani ya taifa. Nilikuwa na mgogoro kidogo na utawala kwa kuwa labda serikali ya Mwalimu Julius Nyerere ilifikiria kuwa kitabu changu kitapingana na mfumo wetu mpya wa Ujamaa. Walinijia maafisa wa polisi na vijana wa usalama wa taifa na kunihoji wakitaka kujua madhumuni yangu katika kutoa kitabu cha ‘kisiasa’. Niliwajuza kuwa hata sikuwa na habari kuwa azimio la azimio lipo au litatoka lini? Viongozi wengi serikalini hawakukipenda sana kwa kuwa

Mbona kazi zako nyingi zinaelekea kutetea haki za umma na kupinga dhuluma katika jamii?

Kwa kweli mimi napenda siasa sana. Nimewahi kuwa diwani wa Manispaa ya Bukoba miaka ya 1980 na hata baadaye nikajaribu kugombea ubunge ila nikaibuka wa tatu mwakani 1985. Sidhani hadi wa sasa kama nilishindwa kihalali. Ninaona siasa kama njia moja ya kutoa uongozi na kuelekeza jamii na kufikia hadhira kubwa. Siasa sasa zimegeuzwa jukwaa la kujichumia mali kwa urahisi. Hata nimeangazia dhuluma katika jamii katika  kazi zangu kama ‘Sayari iliyozama’ ambapo nilitumia ndege kuonyesha uozo wa kimaadili  kama ulaji rushwa na wizi  wa kura uchaguzini na kadhalika. Mathalan, riwaya ya Shamba la Wanyama ni kioo cha uhalisia ulioko katika serikali zetu hasa barani Afrika ambapo viongozi wanaanza kwa lengo moja la kupinga dhuluma lakini hatimaye wakishatwaa hatamu za uongozi, wanabadilika  na kuwa kama watangulizi wao. Yule mhusika nguruwe aliyeitwa Mkimwa riwayani na wengineo kwa mfano ni viwakilisho hakika vya viongozi kama hawa.

Riwaya ya Shamba la Wanyama ilisomwa sana Kenya au Tanzania?

Kusema ukweli, kilishamiri sana nchini Kenya kuliko hapa Tanzania. Mauzo yake hadi wa sasa nchini Kenya ni ya kufurahisha. Kimekuwa kikisomwa kama riwaya teule nchini Kenya kwa miaka mingi. Labda ni kwa sababu palitoa mwamko mpya wa kisiasa na kijamii nchini Kenya kabla ya Tanzania kwa kuwa sisi hapa tulilimatia katika siasa za kujitegemea za Ujamaa. Utamaduni wa kusoma ulikita mizizi Kenya kuliko Tanzania.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuathiri kwa njia yoyote katika uandishi wa wako?

Mwanzo mimi nilishuhudia Tanganyika ikijinyakulia uhuru. Zile hotuba za Mwalimu Nyerere za kwanza na mwelekeo tuliokuwa tumeanza nao ulikuwa  unatia moyo sana. Kidogo kidogo tulianza kupoteza mwelekeo na lengo tuliloanza nalo. Niliposoma  Animal Farm ya George Orwell nikaanza kung’amua kuwa  kumbe haya ninayoyasoma riwayani inaelekea ni kama yanayoanza kutokea nchini. Hilo likanisukuma kuharakisha kukitoa kitabu hiki. Pia uhalisia wa mambo nchini Tanzania wakati huo ulinisaidia kutafuta majina ya wahusika katika Kiswahili.

Je, bara la Afrika katika karne ya 21 limetoka katika ‘Shamba la Wanyama’?

Kwa maoni yangu, hata hali ni mbaya zaidi katika nchi zetu kwa kuwa pengo baina ya tabaka la maskini na matajiri linazidi kupanuka. Viongozi wanaboresha maslahi yao ni kusahau ya umma. Tunashuhudia wabunge wetu wakijiongeza posho na hata mishahara wakati walimu hawalipwe hela zao. Kama nguruwe kina Mkimwa walivyojiongeza maziwa, wanasiasa wanajijaji tu. Uzuri wa mambo ni kuwa kuna demokrasia na uhuru wa kujieleza kuliko siku za mwanzoni. Suluhisho lipo katika kizazi kipya kikipewa nafasi za uongozi . Wafike mahali na wakatae hongo na uozo wowote katika jamii na wajitenge na Waliotangulia.

 

Waandishi kama wewe watabadilishaje jamii na kuiboresha?

Kazi za fasihi zina nafasi kubwa ila pia kuna changamoto kwa kuwa utamaduni na hamu ya kupenda kusoma kazi hizo ili wapate ujumbe. Vipo vitabu vingi vilivyo na ujumbe unaoweza kubadilisha hata mifumo ya kisiasa. Tumejitolea hata kupunguza hata bei za vitabu ili viingie shuleni lakini mwitiko ni mdogo sana. Unashangaa wanafunzi wanaanguka mtihani kwa asilia kubwa kwa kukosa kusoma. Pia mifumo ya elimu inahitaji mabadiliko. Wizara ya elimu ina jukumu la kuwaridhirisha walimu na kutoa mitalaa inayoambatana na maendeleo katika jamii. Vitabu sibakia kama biashara tu.

Sasa unajishughulisha na nini?

Mimi bado nazidi kuandika vitabu. Hivi karibuni nitatoa tamthilia yangu. Aidha ninafanya kilimo katika shamba langu pamoja na ufugaji. Hali kadhalika ninatoa mchango wangu katika jamii ya Bukoba kama mjumbe wa Baraza la Ardhi na Nyumba nikiwa mmoja wa washauri. Pia mimi  mwenyekiti wa chama cha SACCO ya kata ya Kibeta na vikundi vinginevyo. Pia ninashiriki katika shughuli za UKUTA kama Katibu wake. Ukuta ni Chama cha Usanifu wa Kiswahili na Ushairi -UKUTA- ambacho kimeshirikiana na BAKITA-Baraza la Kiswahili la Taifa na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili- Chuo Kikuu cha Dar es Salaam-TATAKI katika kuandaa hafla hii ya kumuenzi Shaaban Roberts.

 

Hezekiel Gikambi ni mtaalamu wa lugha ya Kiswahili na Tafsiri na pia Meneja wa Mradi wa Swahilihub.com wa Nation Media Group, Nairobi Kenya na mwandishi wa Safari ya Serengeti.

Barua pepe: hezekielgikambi@gmail.com

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment

Book Review Guru: A Long Walk to Success by Narendra Raval - A Testament to Grit, Purpose, and Unyielding Faith Reviewed by Hezekiel G...